
Wasanii Diamond Platnumz, Lady Jaydee na Ali Kiba waliacha gumzo mwishoni mwa wiki wakati walipotumbuiza katika hafla maalum iitwayo Club E Hollywood Glam Night iliyofanyika katika ukumbi wa Ubungo Plaza.Katika hafla hiyo ambayo ukumbi ulipambwa kwa mandhari kama ya Hollywood ya Marekani, wanachama wa Club E na wageni wengine waalikwa walipata burudani ya aina yake kutoka kwa wasanii hao wa Kitanzania. Wasanii wote waliotumbuiza walivaa kama wasanii wa Hollywood na pia kulikuwa na picha mbalimbali wasanii nyota wa Hollywood na michezo mbalimbali ambayo ilichangamsha mandhari hayo. Kulikuwa pia na sehemu za kupiga picha na mavazi kama yanayovaliwa Hollywood, gurudumu la bahati yaani ‘wheel of fortune’ na pia wageni waalikwa walipata nafasi ya kushinda zawadi mbalimbali. Msanii wa kwanza kupanda jukwaani alikuwa Judith Wambura maarufu kama Lady Jaydee ambaye aliimba nyimbo saba mfulululizo na bendi yake ya Machozi kabla hajapanda Ali Kiba. Wakati Kiba akiwa jukwaani, Jaydee alipanda tena na wakafanya onyesho la pamoja kwa kuimba wimbo wa Kiba wa ‘Single Boy, Single Girl’ huku mashabiki wakishangilia jinsi wasanii hao walivyotumia vipaji vyao vizuri. Yoyote aliyeona jinsi wasanii walivyovalia hakushindwa kugundua kwamba ulikuwa ni Usiku wa Hollywood ndani ya Jiji la Dar es Salaam. Ukumbini pia kulikuwa na picha za wacheza filamu maarufu kama Denzel Washington, Will Smith, Samuel L Jackon na Angelina Jolie. Makundi mawili ya dansi yenye vijana wenye vipaji, Best Friends na FBI hayakuachwa nyuma kwani vijana hao walitoa burudani ya aina yake na kuwafanya mashabiki kutaka zaidi. Naye msanii Diamond Platnumz hakuwaangusha mashabiki wake kwani alipopanda jukwaani aliwasha moto mwanzo hadi mwisho kwa nyimbo na uchezaji wake pamoja na madansa wake huku mashabiki pia wakiimba na kucheza. Baadhi ya watu waliohudhuria, waliwapongeza waandaaji wa hafla hiyo ya aina yake hasa kwa kuthamini wasanii wa ndani ambao walitoa burudani ya aina yake bila kusahau chakula chenye ubora wa hali ya juu ambacho kilipatikana kuanzia mwanzo hadi mwisho wa shughuli. Club E, iliyoanzishwa mwaka 2007 na ina wanachama zaidi ya 2000 kote nchini, huandaa shughuli mbalimbali za burudani hususan kwa wanachama wake na wageni waalikwa kila mwaka.