MENU

Friday, June 8, 2012

Awamu ya pili kampuni 100 bora yazinduliwa

 













Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Tido Mhando akizungumza kwenye uzinduzi wa Awamu ya Pili ya Tathmini ya Kampuni 100 za Daraja la Kati, zinazokua kwa haraka, uliofanyikajijini Dar es Salaam

KAMPUNI ya Mwananchi Comunications Ltd  (MCL) ikishirikiana na KPMG Tanzania wamezindua awamu ya pili ya tathmini ya kampuni 100 za daraja la kati, zinazokua kwa haraka ili kuonyesha ubora wao katika biashara na mafanikio.
Washindi wa tathmini hiyo watatangazwa Oktoba mwaka huu na washiriki watafaidika na fursa ya kupata wabia muhimu na wazoefu ili kuboresha biashara zao.
Uzinduzi huo ulifanyika Jijini Dar es Salaam jana ambapo Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Raymond Mbilinyi alisifu mpango huo akisema utaisaidia Serikali kutunga sera itakayokuza uchumi wa nchi.
“Zoezi hili litasaidia Tanzania kutengeneza sera,” alisema Mbilinyi akifafanua kuwa Serikali ipo kwenye mchakato wa kutathmini mchango wa wajasiriamali hao wa kati katika uchumi.

Alizielezea kampuni za daraja la kati kuwa zinachangia asilimia 30 ya pato la taifa na zinaajiri Watanzania 2.7 milioni na kushika nafasi ya pili kisekta baada ya kilimo.
Mbali na hilo, Mbilinyi alisema tathmini ya wataalamu wa uchumi inaonyesha nchi zilizopata maendeleo ya haraka duniani ni zile ambazo kampuni za daraja la kati ziliendelezwa vizuri na kukua kwa haraka.

Hivyo, akazitaka kampuni nchini kutumia fursa ya tathmini ya kampuni bora 100 inayoendeshwa na MCL pamoja na KPMG ili kupata fursa ya kujifunza na kupata maarifa ya kujikuza kwa haraka.

“Hata kampuni kubwa zenye mafanikio makubwa duniani kwa sasa kama vile Microsoft, Google na Volkswagen zilianza kama kampuni ndogo… Mafanikio yake yanatokana na kutumia kikamilifu fursa za kujikuza,” alidokeza Mbilinyi.

Aliweka wazi kuwa kukua kwa kampuni za daraja la kati kutasaidia kuongeza ajira na pato la taifa, hivyo kujenga uchumi wa nchi unaokua kwa haraka.

Mkurugenzi wa KPMG Afrika Mashariki, David Gachewa alielezea sifa za kampuni zitakazoshiriki kuwa ni zile zenye mapato kati ya Sh1 bilioni hadi Sh20 bilioni.

Sifa nyingine ni kuwa na kumbukumbu za ukaguzi wa fedha kwa miaka mitatu na zisiwe zimejiorodhesha kwenye soko lolote la hisa.
Mchakato wa kukusanya takwimu za washiriki, alisema utaanza Juni 21, mwaka huu na kwamba wigo umepanuliwa zaidi kwa kutoa fursa kwa kampuni kutoka maeneo mbalimbali nchini kushiriki.Gachewa alisema baada ya tathmini washiriki wote watapata mrejesho kuhusu utendaji kazi wao ili kujipanga katika kuimarisha biashara.

Gachewa alisema tathmini yao haitajitajikita kwenye taarifa watakazotumiwa na washiriki na badala yake timu yake itazitumia tu katika kuwawezesha kufanya uchunguzi wa kina.

Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Tido Mhando alisisitiza kuwa tathmini yao itafanyika kwa umakini na siri kubwa na mshindi atafahamika katika siku ya mwisho watakapomtangaza.

Alisema MCL ambayo ndiyo inayoandaa na kuchapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti, imeamua kuendesha tathmini na mashindano hayo kwa lengo la kuimarisha uchumi wa Tanzania.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Uhandisi ya BQ, ambayo iliibuka mshindi katika tathmini ya mwaka jana, Injinia John Bura alisifu mashindano hayo akisema yameipa Kampuni yake dira na hamasa ya kukua zaidi.“Kampuni yangu imejifunza mengi… nashukuru Mwananchi Communications (Ltd) na KPMG kwa kuandaa mashindano haya… nazihamasisha kampuni nyingi nazo zishiriki ili ziweze kufunguka zaidi,” alisema Injinia Bura.