
KOCHA Mfaransa, Mankour Boualem aliyeifikisha FC Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwenye Nane Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2010 amewaambia Yanga wampe kazi awaonyeshe utamu wa mafanikio yake na kazi ya kwanza itakuwa kuipeleka Yanga kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mankour, ambaye kwa sasa yupo kwao Ufaransa tayari ameshawasiliana na uongozi wa Yanga kupitia kwa straika wa zamani wa timu hiyo, Patrick Katalay ambaye amewaambia kwamba ni bonge la kocha na ana uzoefu na soka la Afrika.
Mbali na kocha huyo ambaye anasubiri simu ya Yanga atue nchini kwa majadiliano ya mkataba kuziba pengo la Kosta Papic, Katalay pia atailetea Yanga wachezaji watatu ambao ni mastraika wawili na beki mmoja wa kati.
Mankour Boualem(41) alizungumza na Mwanaspoti jana Jumatatu kutoka Ufaransa na kusema kuwa anataka nafasi ya kufanya kazi na Yanga kwavile anadhani kuna mazingira mazuri ya kupiga hatua kisoka ndani na nje ya nchi.
Kocha huyo alisema;
"Natamani sana kufanya kazi na Yanga African na kuipa mafanikio stahiki katika kiwango cha kitaifa na kimataifa, nina malengo makubwa sana na ninajua soka la Kiafrika lilivyo, wakikubali kunipa nafasi nitabadili sana mambo hapo na kila mmoja atafurahi, waambie wanipe hiyo timu.
Lengo langu ni kuwapeleka mpaka fainali ya Afrika."
Mankour ambaye anazungumza kiufasaha lugha ya Kingereza, Kiarabu, Kireno na Kifaransa amefanya kazi Morocco, Tunisia, Uturuki, Ufaransa.
Kocha huyo amefanya kazi na Lupopo tangu mwaka 2007 mpaka 2010 kwa vipindi tofauti ambapo na kuipa ubingwa mara mbili kwenye jimbo la Katanga lililopo Lubumbashi, DRC. Mafanikio makubwa zaidi ya Kocha huyo ni kutinga hatua ya nane bora ya Ligi ya Mabingwa msimu wa 2010 na amekuwa akitumia mfumo wa 4-3-3 kila anapokuwa ambapo aliondoka Lupopo kwa matatizo ya masilahi. Katalay aliiambia Mwanaspoti kuwa;
"Tulishazungumza na Yanga wakasema tusubiri kwanza mambo yakae sawa klabuni, ila huyo kocha yuko tayari muda wowote na kwa Yanga ninayoijua mimi ataiweza, ana uzoefu sana na mazingira ya Afrika mimi nimefanya naye kazi sana pale Lupopo, namjua sana Yanga wakimpa nafasi atawasaidia."
Katibu wa Yanga, Selestine Mwesigwa aliiambia Mwanaspoti jana Jumatau kuwa; "Kuna makocha kama 21 wameomba kazi, huyo Mfaransa ni mmoja wao na kila mmoja bado ana nafasi ya kupata, tukikutana kujadiliana tutaamua lakini bado hatujafanya maamuzi."
Timu alizopitia kocha huyo.
2009/10- FC Lupopo DRC
2009 � Avenir Sportif Gabes daraja la pili Tunisia
07/09 -FC Lupopo DRC
2006 � Sakaryaspor daraja la pili Uturuki
2005 - K�nitra ya daraja la pili na kocha wa mradi wa vijana wa Morocco
2004/05 - La Vitr�enne CFA ya Ufaransa kama msaidizi
2002/04 - AS St Jacques DRH ya Ufaransa
2001/02 - Stade Rennais FC U 17 ya Ufaransa
2000 - Noyal Chatillon PH ya Ufaransa
96/98 - Clermont FC daraja la Ufaransa na kocha U 15 ya nchi hiyo.