MENU

Thursday, June 7, 2012

Taasisi ya Mkapa yakusanya 3.2bn/-kupambana na ukimwi

Rais Jakaya Kikwete (katikati) akiwa na marais wastaafu, Benjamini Mkapa (kushoto) na Ali Hassan Mwinyi, wakati wa harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya Programu ya Mkapa Fellows,
 Taasisi ya Mkapa Foundation imefanikiwa kukusanya Sh. bilioni 3.2 kupitia harambee iliyofanywa kwenye hafla ya chakula cha jioni iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Kiasi hicho cha fedha kimepita lengo lililokusudiwa la kukusanya Sh. bilioni 3 kupitia programu ya Mkapa Fellows ambayo inalenga kuendesha miradi ya kusaidia huduma za afya nchini, hasa maeneo ambayo huduma hizo ni hafifu.

Huduma hizo zimejikita zaidi katika maeneo matatu: kuimarisha huduma kwa waathirika wa virusi vya ukimwi (VVU), huduma za afya kwa ujumla hasa kwa kinamama wajawazito na watoto na kuimarisha mifumo ya taasisi katika sekta hiyo.

Fedha zilizopatikana kwenye harambee hiyo zilitolewa na watu mbalimbali baada ya kuhamasika na kuguswa na jinsi Taasisi ya Mkapa Foundation inavyosaidia na kuokoa maisha ya  Watanzania wengi vijijini.

Mgeni rasmi kwenye harambee hiyo alikuwa Rais, Dk. Jakaya Kikwete,  ambaye alishirikiana na marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa.

Vitu mbalimbali vilinadiwa kwenye harambee hiyo zikiwepo picha za marais hao walioingoza Tanzania kwa awamu tofauti tangu mwaka 1985.

Kabla ya kuanza mnada huo, tayari watu binafsi, mashirika na makampuni mbalimbali yalihamasika na kuchangia Sh. bilioni 1.5 ambazo zilikuwa ni nusu ya makadirio.

Mmoja wa wahamasishaji na kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, alisema Rais Mkapa amekuwa akishawishi wahisani wa nje waisaidie taasisi hiyo kufanikisha mikakati yake lakini safari hii ameona ni vyema Watanzania wenyewe wakachangia.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji wa Taasisi ya Mkapa Foundation, Dk. Ellen Senkoro,  alisema mchango huo wa hisani ni bajeti ya mwaka mmoja katika kutekeleza mpango wa miaka mitano wenye lengo la kuchangia jitihada za serikali kupambana na ukimwi, kuzuia vifo vya kinamama na watoto ili kutimiza malengo ya milenia namba nne, tano na sita.

Alisema mradi huo mzima utagharimi shilingi bilioni 15.

Naye Rais Kikwete, alisema pamoja na juhudi kubwa za serikali za kuimarisha huduma za afya nchini, bado huduma hizo hazijafikia kiwango kinachotakiwa kama inavyopendekezwa kitaalam.

Aliisifu Taasisi ya Mkapa kwa juhudi zake za kupunguza tatizo hilo huku akiwahamasisha watu mbalimbali waliohudhuria kuchangia ili kuleta matumaini kwa Watanzania, hasa waishio vijijini.