
Mrembo atakayefanikiwa kuibuka mshindi katika shindano la Miss Dar Intercollge mwaka huu ambalo linafanyika leo Ijumaa kwenye ukumbi wa Makumbusho ya Taifa uliopo mkabala la Chuo cha usimamizi wa fedha (IFM), atazawadiwa fedha taslimu Sh. 500,000 pamoja na gauni lenye thamani ya Sh. 500,000 kutoka kwa mbunifu maarufu wa mavazi nchini, Mustafa Hassanali.
Mratibu wa shindano hilo, Dina Ismail, alisema jana kwamba maandalizi ya shindano hilo litakalopambwa na mshindi wa tuzo tatu za Kili Music Nassib Abdul ‘Diamond’ yamekamilika ambapo warembo 14 kutoka vyuo mbalimbali watachuana.
Alisema mshindi wa pili atazawadiwa Sh. 350,000 wakati mshindi wa nne na wa tano kila mmoja atazawadiwa Sh. 200,000, huku washiriki watakaosalia kila mmoja atapata kifuta jasho cha Sh.150,000.
Aliwataja warembo watakaochuana kuwania taji hilo kuwa ni pamoja na Neema Michael(CBE), Jamila Hassan (DSJ), Natasha Deo, (Ustawi), Diana Nyakisinda (DSJ), Saada Seleman, Rose Masanja (Ustawi), Sharifa Ibrahim (DSJ), Nancy Maganga (Ustawi), Rose Mushumbushi (CBE), Veronica Yolla (DSJ), Veronica Ngota (CBE), Jaquline Cliff (DSJ), Catherine Christian (OUT) na Hilda Edward (Ustawi).