Wasio wajumbe yaani watumishi kutumia bilioni 4.3/-
Sh bilioni 2.0 kulipia nyumba wafanyakazi wa Sekretariati
Jaji Joseph Warioba
Iliyopewa jina la Vote Number 8 (Fungu namba 8), wajumbe 34 wa tume hiyo wametengewa posho ya Sh. bilioni 10 watakayolipwa kwa kipindi cha mwaka mmoja jambo ambalo baadhi ya wabunge wamesema hawaridhiki na kuhoji serikali inatafuta kitu gani kwa tume hiyo.
Wajumbe wa kawaida wa tume hiyo kwa mujibu
wa mchanganuo wa bajeti, watalipwa posho ya Sh. karibu 450,000 kwa
siku lakini Makamu Mwenyekiti na Mwenyekiti wa Tume fungu lao ni kubwa
zaidi ambalo limeongezewa viburudisho na takrima.
Kwa mujibu wa taarifa za uchambuzi wa
posho hizo, kila mjumbe kuanzia mwaka wa fedha wa Julai 2012 hadi Julai
2013, atakuwa amejikusanyia zaidi ya Sh milioni 294 jambo ambalo
baadhi ya wabunge waliohojiwa na NIPASHE Jumapili walisema ni maajabu ya
Firauni.
Pamoja na kuhakikishiwa kuwa na ukwasi
mkubwa, pia wametengewa Sh. milioni 10 kwa ajili ya matibabu kwa wale
ambao wameelezwa kuwa hawapo kwenye utaratibu wa kugharamiwa tiba na
serikali.
Dau kubwa ambalo lipo kwenye bajeti hiyo
kwa mujibu wa wabunge hao ambao wameomba majina yao yasitajwe, ni
kutengwa Sh. milioni 250 zinazodaiwa zitatumika kwa ajili ya usafi na
ulinzi wa ofisi za Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Wajumbe hao 34 kutoka Bara na Visiwani
wametengewa Sh milioni 10 kugharamia mazishi na kuwasafirisha wajumbe wa
tume hiyo watakaofariki dunia wakati wakiwa kwenye mchakato wa
kukusanya maoni.
Sambamba na hilo, tume hiyo imetengewa
zaidi ya Sh. bilioni 10 kununua magari 56 ambayo sita kati yake ni Land
cruiser heavy duty zenye mikonga zitakazofungwa vipaza sauti ili
kukusanya watu watoe maoni yao na mengine 50 yatakuwa ni mashingingi ya
kisasa maarufu kama V8. Kwa sasa tume hiyo inadaiwa kuazimwa magari
kutoka Wizara ya Sheria na Katiba.
Baadhi ya wabunge waliliambia gazeti hili
kuwa bajeti na idadi ya magari imepunguzwa badala ya kutumia Sh. bilioni
10 zitatumika Shilingi bilioni sita na kwamba yatakayonunuliwa ni
magari 26 badala ya 56 lakini idadi ya Land cruiser heavy duty
zitakazofungwa vipaza sauti haijabadilika.
Ofisi ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba pia
inatarajiwa kutumia Sh milioni 256 kugharamia umeme na maji ambapo kila
huduma imepangiwa kugharimu karibu Sh milioni 128, yaani umeme Sh.
127,992,000 kadhalika maji nayo yamepangiwa kugharimu kiasi hicho na
kuwafanya wabunge wachambuzi kuhoji sababu za gharama za umeme na maji
kufanana.Tume hiyo imetengewa posho ya takrima iliyoitwa hospitality services ya
jumla ya Sh. milioni 300 huku simu za TTCL pamoja na gharama za nukushi
(fax) zikifikia karibu Sh. milioni 127 wakati zile za mkononi
zitawagharimu walipa kodi zaidi ya Sh. milioni 91.2.
WAFANYAKAZI WA SEKRETARIATI YA TUME
Kundi hili sio la wajumbe bali hawa ni
watumishi wa ofisini watawala, wahasibu, makatibu muhtasi, wafagizi,
wataalamu wa kompyuta, madereva na wengine nao wametengewa mafungu
kadhaa ikiwemo posho ya kujikimu wakisafiri nayo ni Sh bilioni 4.3.
Kingine ambacho wabunge waliochambua Vote
No 8 ama fungu hilo walisema kilichowashangaza ni kutenga Sh bilioni
2.0 kwa ajili ya kulipia nyumba za wafanyakazi wa Sekretariati ya Tume
na kuhoji hivi wafanyakazi hao hawana nyumba jambo lililoelezewa na
wawakilishi hao wa wananchi kuwa ni ulaji ambao wanasubiri kuuhoji
wakati serikali ikiwasilisha bajeti hiyo.
Pia wafanyakazi hao ambao watalipwa posho
ya Sh. 50,000 kwa siku wametengewa Sh. milioni 300 kwa ajili ya
kununulia vifaa vya chai ambavyo havikuelezwa ni vitu gani pamoja na
vitafunwa. Tume ya Mabadiliko ya Katiba inaongozwa na Jaji Joseph
Warioba ambaye ni Mwenyekiti wakati Makamu Mwenyekiti ni Jaji Augustine
Ramadhani.